MKURABITA ni nini?

Chimbuko la sekta isiyokidhi matakwa ya sheria au sekta isiyo rasmi
Kukua na kushamiri kwa sekta isiyokidhi matakwa ya nchini ni matokeo ya mtiririko wa matukio mbalimbali ya kihistoria. Wakati wa ukoloni sheria na taratibu zilizotumika ziliwanyima wazawa fursa ya kumiliki mali kisheria kama vile ardhi na kuruhusu watu wachache hasa raia wa kigeni kumiliki mali na kufanya biashara katika mfumo rasmi. Taratibu hizi zilichangia kuwepo kwa mifumo miwili ya kumiliki mali na kufanya biashara, ambapo raia wa kigeni wliendesha shughuli zao katika mfumo rasmi na wazawa waliendelea kumiliki rasilimali katika mfumo usio rasmi. Mifumo hii imeendelea hata baada ya jitihada za serikali za kuunganisha njia kuu za uchumi na uzalishaji chini ya mfumo mmoja wa umma kupitia Azimo la Arusha la mwaka 1967.

Katika jitihada za kuhakikisha kuwepo kwa mfumo wenye usawa na manufaa kijamii na kiuchumi kwa wananchi walio wengi, Serikali ya Tanzania ilitekeleza maboresho ya kiuchumi ambayo yalileta matokeo mazuri kiuchumi katika ngazi ya taifa. Pamoja na mafanikio hayo, maborsho hayakuweza kuwanufaisha moja kwa moja Watanzania walio wengi ambapo karibu Asilimia 30 wanaishi katika umasikini uliokithiri. Utekelezaji wa maboresho haya katika miaka ya 1995-2005 umeonyesha kuwa mfumo usio rasmi katika umiliki wa rasilimali na uendeshaji wa biashara ni kikwazo kikubwa katika jitihada za kupunguza umasikini na kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa Watanzania walio wengi.

Kuendelea kuwepo kwa sekta isiyo rasmi nchini kunatokana na sababu mbalimbali ambazo ni pamoja na; wingi wa mifumo ya kitaasisi, vikwazo vya kisheria; gharama za ufuatiliaji wakati wa kurasimisha rasilimali au biashara; pamoja na vizuizi vya kiutawala. Kutokanan na vikwazo hivi watanzania wengi walio katika mfumo usio rasmi wamejiundia mifumo, kanuni na taratibu mbalimbali wanazozitumia katika kufanya biashara ba kupata haki miliki ambazo hazitambuliwki kisheria

Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA)
Kwa kutambua mchango mkubwa unatolewa na wananchi wanaoendesha shughuli za kiuchumi katika sekta isiyo rasmi, Serikali ya Tanzania ilianzisha Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kwa lengo la kuweka mifumo ya kisheria na kitaasisi yenye gharama nafuu na inayoweza kufikiwa na kutumiwa na watu wengi zaidi katika mchakato wa kurasimisha rasilimali na biashara.

 

 

 
 
  • Hakikisha kuwa mipaka ya kijiji imehakikiwa na kupimwa ipasavyo ili kuepusha migogoro ya mipaka na vijiji jirani
  • Kijiji kiwe kimesajiliwa na kupata Cheti cha Ardhi ya Kijiji
  • Kijiji kiwe na jengo linalofaa kwa Masjala ya ardhi ya Kijiji
  • Maombi ya kupimiwa na kupata hati miliki ya kimila yapelekwe kwenye Halmashauri ya Kijiji kwa ajili ya mapendekezo ya kuidhinishwa
  • Maombi lazima yapitishwe na kuidhinishwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji
 
 
  • Kutambuliwa na kuainishwa kwa eneo la urasimishaji na Halmashauri husika katika mji, Manispaa au Jiji,
  • Uhamasishaji kwa Uongozi na wananchi wa eneo la urasimishaji,
  • Utayarishaji wa michoro ya mipango miji na kuidhinishwa na mamlaka husika,
  • Upimaji ardhi ya wananchi kulingana na michoro ya mipango miji
  • Uidhinishaji wa ramani za upimaji kwenye mamlaka husika,
  • Utayarishaji na utoaji wa Hati za kumiliki ardhi kwa wamiliki wa ardhi iliyopimwa.