Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), ambao utekelezaji wake umegawanyika katika awamu kuu nne, mnamo Mei 2008 Timu ya wataalam wa maboresho ilifanikiwa kukamilisha Awamu ya Pili ya Uandaaji wa Maboresho. Awamu hii ilifuata mara tu baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza iliyolenga katika kubaini ukubwa wa sekta isiyo, thamani ya uchumi ulio katika sekta hiyo pamoja na vikwazo na vivutio vinavyowafanya wamiliki wa rasilimali na biashara waendelee kubaki katika sekta hiyo.
Kazi ya kuandaa Mapendekezo ya Maboresho alianza Januari 2006 ikiwa imejikita zaidi katika kuweka misingi imara ya kiutawala ya kurasimisha rasilimali na biashara ambayo inaendana na mifumo ya kijamii kama ilivyobainishwa katika tathmini.
Awamu ya Pili pia ililenga katika kutoa mapendekezo ya maboresho ya kisera, kisheria na kitaasisi pamoja na mbinu za jinsi ya kutekeleza mapendekezo ya maboresho yatakayowezesha mchakato wa urasimishaji wa rasilimali na biashara kuwa wa kasi na gharama nafuu. Nia ikiwa ni kuwawezesha wananchi wanaomiliki na rasilimali na biashara kuingia katika sekta rasmi ili kuweza kuchangia katika shughuli za ukuaji wa uchumi, kuongeza kipato na hatimaye kupunguza umasikini.
Lengo na madhumuni ya Uandaaji wa Maboresho zaidi ilikuwa ni kuondoa vikwazo kama ilivyobainika katika Tathmini ya Sekta isiyokidhi matakwa ya kisheria (extra legal sector), hivyo timu ya MKURABITA na wadau wake walizingatia zaidi maeneo makuu matano ambayo ni:
- Kuhakiki taarifa za uchambuzi wa mifumo ya kijamii isiyo rasmi kama ilivyobainishwa katika tathmini ya awamu ya kwanza:
- Kufanya tathmini ya kuandaa mfumo mpya utakaojumuisha mifumo isiyo rasmi ya kumiliki na kufanya biashara katika sekta isiyo rasmi na mifumo rasmi ya kisheria na kitaasisi:
- Kujifunza kupitia maboresho na mipango inayoendelea:
- Kujifunza kutokana na miradi ya majaribio inayoendelea: na
- Kuoanisha mipango ya maboresho, sera na mikakati mingine ya kitaifa.
MKURABITA yanajumuisha maeneo makuu matano ya mapendekezo ya maboresho ambayo utekelezaji wake utawawezesha wamiliki rasilimali kutambulika kisheria na kutumia rasilimali hizo kujinufaisha kiuchumi katika mifumo ya uchumi wa soko. Matokeo mengine yaliyopatikana katika awamu ya pili ni pamoja na uandaaji wa mkakati wa mawasiliano na mpango kazi wake; tathmini ya faida zinazothibitisha umuhimu wa kuwekeza katika mpango huu; na mpango wa ufuatiliaji na thathmini ya mchakato mzima
Hivyo katika mchakato wa Maandalizi ya Maboresho maeneo makuu matano yamependekezwa na MKURABITA ili kutoa mfumo bora wa sera, sheria pamoja na mfumo wa kitaasisi katika kutekeleza Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania. Maeneo haya ni pamoja na:
- Maboresho yatakayowezesha urasimishaji wa rasilimali na biashara nchini kwa haraka na gharama nafuu.
- Maboresho yatakayowezesha matumizi ya mchakato wa kuziunganisha rasilimali zisizo rasmi na matumizi ya kiuchumi kuwa wa haraka na gharama nafuu.
- Maboresho yatakayowezesha urasimishaji wa biashara kuwa wa kasi na gharama nafuu Tanzania.
- Maboresho yatakayowezesha kukua kwa biashara na kutumia mali za biashara kiuchumi
- Maboresho yatakayolenga masuala mtambuka kama vile, vitambulisho vya watu binafsi, kurahishishwa kwa masuala ya kiutawala, kuundwa kwa taasisi itakayoshughulikia urasimishaji wa rasilimali na biashara.

Posted: 8th Jun 10 by MKURABITA
|