Tanzania emblem

The United Republic of Tanzania

Property and Business Formalization Program

News

WAKULIMA KATIKA HALMASHAURI 63 WAFAIDIKA NA MKURABITA


Zaidi ya Sh Bilioni 28.5 zimekopeshwa na taasisi mbalimbali za fedha kwa wakulima waliorasimisha mashamba yao kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) katika halmashauri 63 nchini.

Meneja wa Mkurabita anayeshughulika na urasimishaji ardhi vijijini, Aunthony Temu alitoa taarifa hiyo leo wakati mpango huo ukiwajengea uwezo wakulima wa halmashauri ya Wilaya ya Kilolo waliorasimisha mashamba yao. "Leo tunafanya mafunzo ya namna ya kutumia hatimiliki za ardhi za kimila- kiuchumi, na tunataka mpate mitaji ya kufanya kilimo biashara, ili muondokane na kilimo cha kijikimu kwa hiyo tutawaunganisha na taasisi mbalimbali za fedha, ili mkapate mitaji hiyo na kufanya kilimo chenye tija," alisema. Alisema zaidi ya mashamba 1,330 katika vijiji nane vya Lukani, Lusing'a, Ilamba, Magome, Ng'ang'ange, Kidabaga, Udekwa na Ukwega yamepimwa na wamiliki wake wamepatiwa hati. Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa,

Elinaza Kiswaga alisema; "Lengo la MKURABITA katika mwaka wa fedha 2021/2022 lilikuwa kupima mashamba 1,083, lakini limevuka hadi 1,338." Pamoja na kupima mashamba hayo Kiswaga alisema, Mkurabita umetumia zaidi ya Sh Milioni 60 kuwajengea masjala ya ardhi ya kisasa katika kijiji cha Lukani, ambayo pia ina ofisi za watendaji mbalimbali wa kijiji pamoja na vyumba viwili vya mahabusu.

Akigawa hati kwa walengwa hao, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Peresi Magiri aliupongeza mpango akisema umewawezesha wananchi kutekeleza takwa la kisheria la umiliki wa ardhi, hatua inayotanua wigo na fursa za kujiendeleza kiuchumi sambamba na kumaliza migogoro yao ya ardhi. Naye Kamishna wa Ardhi wa Mkoa wa Iringa, Wenslaus Mtui alisema ardhi ni mali na thamani yake inapanda kwa kadri inavyowekezwa, hivyo ni muhimu kwa wananchi hao kuitumia ipasavyo kujiendeleza na kubadili maisha yao. Mwakilishi wa benki ya NMB Kilolo, John Mtenga, aliwaambia wanufaika hao kwamba benki yao inatoa huduma za kifedha zikiwemo za kujiwekea akiba na mikopo, kwa mtu mmoja mmoja na vikundi. "Tuna fedha nyingi kwa ajili ya kilimo biashara zinawasubirini lakini kabla hamjazipata kwa kupitia mikopo mnayotakiwa kuomba ni lazima muwe na akaunti," alisema huku akiwataka wakulima hao kufungua akaunti katika benki hiyo ili wanufaike na fedha hizo.