Tanzania emblem

The United Republic of Tanzania

Property and Business Formalization Program

History

Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) ulianzishwa kwa Tamko la Rais wa Awamu ya Tatu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa Septemba 2003. Utekelezaji wa MKURABITA ulianza rasmi Novemba 2004 na unafanyika Tanzania Bara na Zanzibar.

Lengo la uanzisha MKURABITA ni kuwawezesha wananchi wanaomiliki rasilimali na biashara nje ya mfumo rasmi waweze kuzirasimisha na kuzitumia kupata mitaji kwa ajili ya kushiriki na kuendesha shughuli katika uchumi wa kisasa unaondeshwa kwa mujibu wa sheria. Mpango huu unalenga kutafuta suluhisho la tatizo la kipekee la rasilimali na biashara za wananchi kutokutambulika kisheria na kutumika kama dhamana ya kupata mitaji na hivyo kutambulika kama mitaji mfu (Dead Capital).

Muundo wa utekelezaji wa Mpango huu, umepangwa kutekelezwa katika Awamu nne (4) ambazo ni: Tathmini ya Sekta Isiyo Rasmi; Maandalizi ya Maboresho ya Kisheria na Kitaasisi; Utekelezaji wa Mapendekezo ya Maboresho; na Ukuaji wa Mitaji na Utawala Bora.

Utekelezaji wa Awamu ya Kwanza uilianza Novemba 2004 hadi Septemba 2005 ambapo ilifanyika Tathmini ili kujua ukubwa na thamani ya Sekta Isiyo Rasmi nchini. Aidha, Utekelezaji wa Awamu ya Pili ulianza Januari 2006 na kukamilika Mei 2008 kwa kuandaa Mapendekezo ya Maboresho ya Kisheria na Kitaasisi yaliyolenga kurekebisha mapungufu yaliyobainishwa kwenye Tathmini ya Sekta Isiyo Rasmi ya mwaka 2005.

Kwa sasa MKURABITA inatekeleza Awamu ya Tatu sambamba na ya Nne ili kuwawezesha wananchi Kurasimisha Ardhi na Biashara na kuzitumia kukuza mitaji ya shughuli zao za kiuchumi.